Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba jana alitoa msimamo mkali kuhusu sakata la escrow na
kwamba ametaka hatua zichukuliwe kwa wahusika wote.
Katika kikao hicho inaelezwa
kwamba Nchemba alionyesha msimamo wake waziwazi kuwa sakata hilo ni
hujuma na kwamba haiwezekani walioiba fedha hizo wakaachiwa tu
hivihivi.
Ndani ya kikao hicho
imeelezwa kuwa Mwigulu alijitokeza na kusema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) ameshamaliza utata hivyo, mali zote, fedha
zote za IPTL zikamatwe na wahusika wote wakamatwe.
Alisema haiwezekani watu
wakawajibika tu kwa kujiuzulu kwa kuwa huko ni kutoa tu likizo mtu akale
mabilioni yake, hivyo wachukuliwe hatua ipasavyo na kufilisiwa.
“CAG ameshasema pesa zile zilikuwa mali ya umma, sasa zikamatwe zote na wahusika wote wakamatwe,” alisema Mwigulu.
Chanzo chetu cha habari
kilieleza kuwa Mwigulu alienda mbali zaidi na kusema hata ambao
walishastaafu na wamehusika kulihujumu taifa wakamatwe na akaunti zao
zikamatwe, zifilisiwe na fedha zirudishwe kwa wananchi.
Pia aliagiza mtumishi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye anatuhumiwa kuchota Sh1.6
bilioni za akaunti hiyo afukuzwe kazi, akamatwe na akaunti zake za fedha
zifilisiwe ili fedha irudi serikalini.
Habari za uhakika kutoka
kikao hicho zinaeleza kuwa Mwigulu aliongea kwa sauti ya mamlaka mbele
ya Waziri Mkuu na kusema kuwa kujiuzulu siyo adhabu stahiki kwa wizi
mkubwa kama huo.
Mwigulu alisema: “Tazama
wanafunzi, watoto wa maskini zaidi ya elfu 40 wamekosa mikopo, madawa
hospitalini hakuna, maskini wanakufa, watu wasio na hatia wanafungwa kwa
kukosa michango ya maabara, walimu wanadai fedha zao, wazabuni
wanauziwa nyumba zao na benki huku wakiidai Serikali kwa huduma
walizotoa, leo wezi tuwape adhabu ya kujiuzulu? Tuwape likizo ya kwenda
kutumia fedha walizo waibia maskini?”
Kwa mtumishi wa TRA aliyekula fedha za IPTL zaidi ya 1.6 bilioni Mwigulu akatoa agizo:
“Nimemwagiza Kamishna wa
Kodi amfukuze kazi yule mtumishi wa TRA iliyoko chini ya wizara yangu na
afilisiwe, pia mitambo na kodi vikamatwe na wahusika wakamatwe.
“Hatuwezi kuendeleza mazoea
ya kufunga maskini na kuwapa likizo wezi wakatumie fedha. Walio
serikalini na walioko kwenye siasa wakamatwe na tuwafilisi fedha irudi
serikalini,” Mwigulu alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment