MKOA
wa Kilimanjaro umepitisha rasmi azimio la kuiomba Serikali kuipandisha
hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuwa jiji ifikapo mwaka 2015.
Azimio
hilo limepitishwa katika kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC), chini ya
Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa, Leonidas Gama ambaye amewataka
watendaji wa ngazi mbalimbali kutekeleza vigezo vichache vilivyobaki ili
kupandishwa hadhi hiyo.
Alisema
miongoni mwa vigezo vikubwa vilivyokuwa vikihitajika ni pamoja na
kuongeza ukubwa wa eneo la Manispaa hiyo kutoka kilomita za mraba 58 za
sasa hadi kufikia kilometa 142, jambo ambalo tayari limetekelezwa.
Alisema
upanuzi wa manispaa hiyo unajumuisha vijiji tisa kutoka Halmashauri ya
wilaya ya Moshi Vijijini na vijiji viwili kutoka Halmashauri ya wilaya
ya Hai ambapo kilomita za mraba 84 zinaongezwa ili kutimia kilomita za
mraba 142 zitazowezesha Moshi kuwa Jiji.
Mkurugenzi
wa Manispaa hiyo, Shaaban Ntarambe alikihakikishia kikao cha RCC kuwa
taratibu zote muhimu zimetekelezwa, ikiwamo elimu kwa wananchi wa vijiji
vitakavyoingizwa katika hadhi ya jiji na kuwaondoa hofu iliyojengwa na
baadhi ya wanasiasa kuwa wanapora ardhi yao.
Kwa
upande wake Meya wa Manispaa ya Moshi, Japhar Michael kwa nyakati
tofauti alikuwa akielezea kuwa mipango ya upanuzi wa Manispaa hiyo
halitahusisha mwananchi kunyang’anywa ardhi na mashamba kama inavyodaiwa
na baadhi ya wanasiasa.
Alisema
mipango hiyo ambayo ina faida kwa wakazi wa manispaa hiyo na wengine
watakaojiunga na jiji hilo, unafanyika kwa kutumia busara na elimu zaidi
kwa wananchi kuliko kutumia mabavu.
Mpango
wa Manispaa hiyo kuwa Jiji uliungwa mkono na Rais Jakaya Kikwete tangu
mwaka 2012 alipofanya ziara mkoani humo ambapo baada ya kuelezwa lengo
hilo alitaka viongozi katika halmashauri husika kukutana ili kuondoa
tofauti zinazojitokeza ili lengo litimie mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment