Ni
wiki ya shida. Wiki hii inatarajiwa kuwa ya vikao mfululizo na mijadala
isiyokoma. Ndiyo wiki inayotarajiwa kuuweka hadharani mtikisiko wa tano
katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wakati ripoti ya uchunguzi wa
sakata la IPTL itakapowasilishwa rasmi kwa wabunge na Taifa kwa jumla
mjini Dodoma keshokutwa na kuhitimisha minong’ono na uvumi.
Ni
wiki ambayo Bunge litaamua juu ya hatua za kuchukua dhidi ya vigogo wa
Serikali ambao wamekuwa wakitajwa kuhusika na ufisadi huo wa kuchota au
kunufaika na Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyoko Benki
Kuu ya Tanzania (BoT).
Ripoti
hiyo inayosubiriwa, itawasilishwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), inayoongozwa na Zitto Kabwe, ambayo itatoa mapendekezo
juu ya hatua za kuchukua.
Wabunge
wa vyama mbalimbali, jana walikuwa na vikao kadhaa wakijipanga jinsi ya
kushughulikia sakata hilo mara tu ripoti itakapowasilishwa.
Wabunge
wa CCM jana jioni walikutana kuwekeana msimamo kuhusu sakata hilo huku
kukiwa na taarifa kwamba baadhi yao, hasa walioonyesha kushabikia ripoti
hiyo, wamekaripiwa na kupewa mwongozo wa kuilinda Serikali.
Habari
za ndani zinasema kuna juhudi kubwa zinafanywa ili kuhakikisha Baraza
la Mawaziri halivunjwi kwa mara ya pili, baada ya tukio la mwaka 2007
alipojiuzulu aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kutokana na kashfa ya
Richmond.
Habari
zaidi zilisema, juzi kilifanyika kikao kingine ndani ya Makao Makuu ya
CCM, Dodoma kikiwahusisha baadhi ya wabunge, mawaziri na vigogo
wanaotuhumiwa katika kashfa hiyo.
Habari
zinasema kikao hicho kilipata muhtasari kutoka ndani ya PAC lakini
hakikufikia mwafaka kutokana na baadhi ya wajumbe kupinga kujadili suala
hilo mbele ya watuhumiwa na bila kupewa ripoti kamili ya Mdhibiti na
Mkaguzi na Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Vilevile,
wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) nao walikutana jana kujipanga kwa ajili ya
kushughulikia sakata hilo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema wameitisha kikao hicho kuwekeana msimamo.
“Tunakwenda
kukutana kama Ukawa ili tuwekeane msimamo jinsi gani ya kulishughulikia
sakata la ufisadi wa Escrow,” alisema Mnyika.
Ripoti
hiyo itawasilishwa huku kukiwa na madai kutoka Ukawa kuwa imevuja na
kusambazwa mitaani na baadhi ya kurasa zenye majina ya wahusika
zikichomolewa ili kuuhadaa umma.
Kurasa
zilizochomolewa zimeelezwa kutawanywa kwa wabunge na mtu mmoja ambaye
Ukawa haujamtaja, lakini ukitaka polisi imshughulikie.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime juzi alithibitisha kumshikilia
mhusika baada ya kumkamata akiwa na nyaraka za Bunge ambazo hazipaswi
kuwa mikononi mwake.
Alisema
walipokea taarifa za mtu huyo kutoka Ofisi ya Bunge na walipomkamata na
kumpekua walikuta nyaraka za aina tatu, mbili zikiwa na muhuri wa
Katibu wa Bunge na alipohojiwa alisema amepewa na mbunge mmoja
aliyeambatana na watu wengine wawili (hakuwataja) ambao bado
wanatafutwa.
Lipumba amvaa Pinda
Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kujiuzulu au kufukuzwa kwa kushindwa kuzuia ufisadi wa fedha katika
akaunti hiyo. Pia amemtaka Pinda awajibike kwa kauli yake kwamba fedha
hizo hazikuwa za umma.
Lipumba
aliwataja vigogo wengine wanaotakiwa kujiuzulu kuwa ni Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi.
Kadhalika,
Profesa Lipumba amevitaka vyombo vya dola kuwakamata na kuwafungulia
mashtaka haraka iwezekanavyo wamiliki wa Kampuni ya IPTL, James
Rugemalira na Habinder Singh Sethi kutokana na kashfa hiyo.
Rugemalira
na Seth wanadaiwa kuchukua Sh321 bilioni kinyume na makubaliano kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ilifunguliwa baada ya kutokea mgogoro wa
malipo kati ya Tanesco na IPTL.
Fedha hizo zilichukuliwa kabla mgogoro huo haujapatiwa suluhisho, kitendo kinachotafsiriwa kuwa kilikuwa na mazingira ya rushwa.
Profesa
Lipumba alisema akaunti ambazo vigogo wa Serikali walipitishia fedha
kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow zinatakiwa kusimamishwa.
Maandamano CUF
Lipumba
alisema chama hicho kwa kushirikiana na wadau wengine wanaandaa
maandamano kulaani vitendo vya kifisadi kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow
na kuwapongeza wabunge walioibua hoja hiyo hadi ukaguzi ukafanywa na
CAG.
Alisema maandamano hayo yatafanyika baada ya mjadala wa siku mbili utakaofanyika bungeni kuhusu sakata hilo.
Alisema baada ya wabunge kujadili watafanya maandamano hayo ili kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusiana na ufisadi huo.
Maaskofu wambana Pinda
Kwa
upande mwingine, Serikali imetakiwa kutoa majibu ya msingi juu ya
sakata la IPTL ili kuepusha minong’ono inayoweza kusababisha uvunjifu wa
amani nchini.
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jakob Chimeledya alisema jana
kuwa suala la escrow limeiweka Serikali katika hali mbaya kiasi kwamba
inaweza isiaminike kwa wananchi wake.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda hakujibu hoja hiyo moja kwa moja
badala yake akasema inapokaribia kipindi cha uchaguzi kunakuwa na mambo
mengi ambayo hujitokeza.
“Mara
nyingi inapokaribia kipindi kama hiki si mnajua mbio zilizoko mbele
yetu? Kwa hiyo kuna mambo yanakuwa ya kweli na mengine siyo ya kweli,
inabidi tuangalie, lakini Serikali itaona namna ya kutoa maelezo,”
alisema Pinda.
Akizungumza
mbele ya mamia ya waumini wa Kanisa hilo katika ibada ya kumweka wakfu
Askofu wa sita wa Dayosisi Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson
Chilongani, Askofu Chimeledya alisema ukimya wa Serikali unatia shaka.
“Tunaitaka
Serikali itoe ukweli kwani sasa Taifa linaishi kwa uvumi tu jambo
ambalo si la kufumbia macho na kama hivi ndivyo hamtaaminika,” alisema
Askofu Chimeledya.
Mwandosya: Hatutaangalia mtu
Wakati
huo huo; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Marc
Mwandosya amesema mbivu au mbichi kuhusu sakata hilo zitajulikana wiki
hii na hataangaliwa mtu, bali masilahi ya chama.
Profesa
Mwandosya alisema hayo jana wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Dodoma ambao ni wafuasi wa CCM waliopata nafasi ya kumhoji
masuala mbalimbali ya chama na Serikali.
Alisema
angependa watu wanaotajwa wajiondoe wenyewe hata kama hawajahusika, kwa
kuwa itakuwa ni nzuri kwao na itakuwa heshima kwa chama... “Hata kama
mtu hajahusika itamsaidia sana akijiondoa kwani italinda chama pia.”
Alisema
kwa kuwa suala hilo linajadiliwa ndani ya vikao vya chama ambavyo naye
huwa anaingia, atatoa ushauri na kuangalia jinsi gani ya
kulishughulikia.
Mbeya na Arusha
Mwenyekiti
Mstaafu na Mwasisi wa CCM mkoani Mbeya, Isakwisa Mwambulukutu ameshauri
watu wote watakaobainika warudishe fedha na kufilisiwa mali zao na kama
ni viongozi wa umma, waachishwe nyadhifa zao zote na wafikishwe kwenye
vyombo vya sheria.
Mbunge
wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amewataka wakazi wa
jimbo lake kutochangia ujenzi wa maabara hadi watuhumiwa waliohusika na
fedha za escrow watakapowajibishwa na kuzirejesha “... huu ndiyo ujumbe
wangu leo hapa Kanisani.”
Alisema
hayo katika ibada ya kusimikwa wachungaji Barakaeli Mungure na Lazaro
Mafie wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa
Mulala.
Nape
Kutoka
Lindi, viongozi wa juu wa CCM wamesema kila mtu atabeba msalaba wake
mwenyewe katika sakata hilo kwa kuwa chama hicho hakiwezi kuwavumilia
viongozi na watendaji wenye nia mbaya na Serikali yake.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema katika mkutano wa
hadhara mjini Lindi jana kuwa, chama hicho ndicho mwasisi wa maadili na
miiko ya uongozi wa umma nchini kuanzia enzi za Tanu, hivyo kitaendelea
kusimamia kwa vitendo dhana hiyo.
Alisema
kinyume na wapinzani wanavyodai kuwa CCM imeondoa kipengele cha maadili
ya umma kwenye Katiba Inayopendekezwa, chama hicho kitaendelea
kuyasimamia bila woga maadili kama kilivyochukua uamuzi mgumu katika
matukio ya Richmond na mengine.
Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema wakati wa kuomba ridhaa kwa
wananchi waliahidi mambo mengi, hivyo ni wajibu wa chama kurudi
kuangalia utekelezaji wake.
Alisema
muda wa kuvumiliana, kubebana na kulindana umekwisha kwani imekuwa
tabia na ugonjwa kwa baadhi ya viongozi kushindwa kusimamia na kukosoa
pale watendaji wanaposhindwa kuwajibika ipasavyo na CCM haiwezi kufumbia
macho mwenendo huo.
Imeandikwa
Boniface Meena, Sharon Sauwa, Israel Mgussi na Habel Chidawali (Dodoma)
Raymond Kaminyoge (Dar), Lauden Mwambona (Mbeya), Mwanja Ibadi (Lindi)
na Mussa Juma (Arusha).
VIA>> MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment