Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akiwasilisha bungeni hotuba ya mwelekeo na malengo
ya makadirio ya matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha
2015/2016, bungeni Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda jana aliwasilisha Bajeti ya lala salama ya ofisi
yake na taasisi zake kwa mwaka 2015/16, huku akieleza mafanikio katika
sekta mbalimbali yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Nne tangu
ilipoingia madarakani mwaka 2005.
Bajeti
hiyo iliwasilishwa katika mkutano wa 20 wa Bunge la 10 ambao ndiyo wa
mwisho kwa Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya Bunge kuvunjwa kuelekea
kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Akitumia
saa 2.30 kusoma hotuba hiyo ya kurasa 105, Pinda alisema katika mwaka
2015/16, ofisi yake imepanga kutumia Sh5.8 trilioni ambazo matumizi yake
yatafafanuliwa katika bajeti za wizara zilizopo chini ya ofisi yake.
Pinda
alitumia fursa hiyo kuzungumzia pamoja na mambo mengine, mafanikio
katika usafirishaji wa reli, bila kugusia harufu ya ufisadi katika
ununuzi wa mabehewa katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) uliosababisha
vigogo wake watano kusimamishwa kazi.
Mafanikio ya Serikali
Pinda
alisema tangu 2005 hadi 2014, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya
uwekezaji, kwamba Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi
7,159 yenye thamani ya Dola za Marekani 74,274 milioni na kutoa ajira
869,635.
Alisema
katika kipindi cha miaka 10, Serikali iliwawezesha wananchi kubaini
fursa za kiuchumi kupitia mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na
kuongeza ajira ulioanzishwa mwaka 2006, kutoa mikopo ya masharti nafuu
ya Sh50 bilioni iliyotolewa kwa wajasiriamali 74,790.
"Katika
mwaka 2015/16, Serikali itaendelea kuwahamasisha wananchi kuanzisha na
kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali, vyama vya kuweka akiba na
kukopa ili waweze kukopesheka," alisema. Kuhusu ajira, alisema vijana
walioajiriwa katika sekta ya umma ni 188,087 na walioajiriwa katika
sekta binafsi ni milioni moja wakati vijana milioni 15 wamejiajiri
katika shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara ndogondogo.
Alisema viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2005 hadi 74 mwaka huu.
Kuhusu
uchumi, Waziri Mkuu alisema umekua kutoka asilimia 4.7 mwaka 2006 hadi
asilimia saba mwaka 2014 na hivyo kuongeza pato la Mtanzania kutoka
Sh360,865 mwaka 2005 hadi Sh1.7 milioni mwaka 2014.
"Uzalishaji
wa mazao ya uvuvi umeongezeka kutoka tani 341,109 mwaka 2006 hadi tani
375,158 mwaka 2015. Tani 43,354 za mazao ya uvuvi na tani 42,100 za
samaki hai wa mapambo ziliuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa Sh7.5
bilioni. Viwanda vya kuchakata samaki vimeongezeka kutoka 25 hadi 48,"
alisema Pinda. Pia, alizungumzia pia sekta ya utalii akisema idadi ya
watalii nchini imeongezeka kutoka 1,095,884 mwaka 2013 hadi 1,102,026 na
kuongeza mapato ya utalii kutoka Dola za Marekani 1,853 milioni hadi
Dola 1,983 milioni.CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment