Na Hassan Abbasi*
Wasomaji na wadau wa maendeleo, kuanzia leo tutakuwa tukiwaletea makala maalumu kuhusu muktadha na utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Kwa kuanzia, leo tutajikita zaidi katika dhana, asili na hoja ya kwa nini BRN imeanzishwa, ili kufahamu ni nini kipya ambacho mfumo huu maalum wa utekelezaji wa miradi unakileta katika utoaji wa huduma za jamii na kukuza uchumi wa nchi.
Ni ukweli ulio dhahiri kuwa mfumo wa BRN, tangu ulipoanza rasmi kutekelezwa Julai mosi 2013, umepokewa kwa hisia tofauti na jamii. Wapo wanaoamini kuwa BRN ni mradi au kaulimbiu yenye taswira za mipango kama hiyo ambayo matokeo yake hayakuonekana vyema.
Wapo ambao hata hivyo bila ya kusubiri kushuhudia na kuona wasiwasi wa kundi la kwanza utakavyojibiwa kivitendo, wenyewe wametuamini moja kwa moja kuwa ukiitazama nia na nira ya BRN ipo haja ya kuamini malengo ya mfumo huu kuwa yatatimia.
Kwetu sisi, hawa wote ni watu muhimu. Walio katika kundi la kwanza wanatupa ari ya kutekeleza na kutimiza malengo, na kundi la pili linatupa moyo wa kutowaangusha waliotuamini. Makala hizi zitalenga kuondoa kiu ya makundi haya yote mawili juu ya muktadha na faida za BRN, ili kila Mtanzania ashiriki katika mageuzi haya.
Muktadha wa BRN
Kwa kifupi, BRN ni kifupi cha maneno ya Kiingereza, Big Results Now, yaani Matokeo Makubwa Sasa. Huu ni mfumo unaoweka vipaumbele, malengo na muda wa utekelezaji, na mfumo wa ufuatiliaji na nidhamu ya kuwajibika kutekeleza malengo hayo kwa ubunifu bila kuendekeza utendaji wa kimazoea.
BRN si kauli mbiu au mkakati au mpango wa kawaida bali ni mfumo maalum wa kisayansi unaosaidia kuharakisha kufikiwa kwa malengo ya kitaifa yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025) pamoja na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Kwa kujikita katika sekta chache za kipaumbele, kuweka malengo yanayopimika katika maeneo machache yenye chachu kwa mengine, na kuweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na muda wa utekelezaji, BRN imeshaanza kuonesha matokeo makubwa. Tutaona baadaye katika makala hizi.
Kwa nini BRN sasa?
Hili ni swali ambalo sisi waumini wa BRN tumekuwa tukikutana nalo mara kwa mara kutoka kwa wadau wetu wa aina nilizozianisha hapo juu. Ujio wa BRN hapa nchini ni matokeo ya vilio vya wananchi na pia tafakuri ya uongozi wa juu na hasa maono ya Rais Jakaya Kikwete katika kutafuta namna bora zaidi ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Tafakuri ni muhimu na ndio maana katika maandiko yake kuhusu “Kujikosoa ni Kujisahihisha,” Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, alipata kusema bila kujitathmini, kujikosoa na kufanyiakazi changamoto Taifa haliwezi kuwa na maendeleo ya maana.
BRN imekuja kuitikia kilio kinachotokana na tafakuri za muda mrefu juu ya hoja na haja ya nchi yetu kuwa na mfumo makini na madhubuti wa utekelezaji wa miradi, sera za maendeleo na mipango mingine yenye tija.
Hoja na haja ya kuwa na mfumo wa kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kitaifa wa aina ya BRN zimeainishwa katika tafiti mbalimbali zinazoheshimka ikiwemo ile ya Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM 2009 na 2013, Ripoti ya Tanzania) na hata mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo yaliyofanyika mwaka 2010.
Langkawi, Malaysia, Juni 20, 2011
Hii ni siku tulivu katika kisiwa cha Langkawi ambapo Rais Kikwete na viongozi wenzake kadhaa wa Afrika walipata fursa adhimu ya kuelezwa uzoefu wa Malaysia katika mabadiliko ya kutoka nchi masikini hadi kuwa nchi ya kipato cha kati.
Itakumbukwa kuwa Malaysia ni nchi ambayo kufikia miaka ya 1960 ilikuwa na uchumi karibu sawa na Tanzania, lakini sasa imepiga hatua kubwa na kujinasua kutoka nchi zinazoendelea na kuingia katika nchi ya kipato cha kati.
Moja ya siri zilizo nyuma ya Malaysia kufikia walipo leo na kuiacha Tanzania kwa mbali ni nidhamu ya utekelezaji wa malengo, sera na mikakati iliyowekwa. Mfumo huu na siri hii ya Malaysia vilisaidia kuleta hamasa iliyomfanya Rais Kikwete kuamua kuchukua mazuri ya mfumo huo na kuingiza uzoefu wa Tanzania ili kuanzisha mfumo wetu wa BRN.
Je, BRN imejengwa katika nguzo zipi zinazosaidia kusukuma mbele utekelezaji wa miradi na mikakati ya kitaifa? Ni namna gani nguzo hizo zimeweza kuwa chachu ya mageuzi nchini. Ungana nami katika safu hii Alhamisi ijayo.
*Makaya haya katika mfululizo wa elimu kwa umma imechapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mwananchi Novemba 20, 2014 na inawekwa hapa kwa hisani ya BRN. Mwandishi ni Meneja Mawasiliano katika Ofisi ya Rais - Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia utekelezaji wa BRN. Kwa maoni, ushauri, wasiliana nasi kwa: simu 0687 222 242; au baruapepe habbasi@pdb.go.tz
0 comments:
Post a Comment