KIPENGA cha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, kinatarajiwa kupulizwa Novemba 30 mwaka huu na uchaguzi kufanyika Desemba 14 chini ya sheria zilizopo.
Taarifa
ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), iliyotumwa katika vyombo vya habari jana, ilifafanua kuwa
uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia masharti ya sheria za serikali za
mitaa na kanuni za uchaguzi huo.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
sheria hizo zimetungwa na ofisi yake, baada ya kuwashirikisha wadau
mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa
kudumu, asasi za kiraia na wadau mbalimbali.
Kwa
uamuzi huo, wagombea wa nafasi zinazowaniwa za mwenyekiti wa mtaa,
kijiji na kitongoji na nafasi za ujumbe wa serikali za vijiji na kamati
za mitaa, wametakiwa wawe wanachama na wadhaminiwe na chama cha siasa
chenye usajili wa kudumu.
Ratiba
Katika
ratiba iliyotolewa sambamba na taarifa hiyo, wasimamizi wa uchaguzi
wameelekezwa kutoa tangazo la majina na mipaka ya mitaa, vijiji na
vitongoji, siku 50 kabla ya siku ya uchaguzi kwa kuzingatia Kanuni ya 6
ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ngazi
ya vijiji, vitongoji na mitaa ya mwaka 2014.
Baada
ya hatua hiyo, wasimamizi hao wa uchaguzi watateua majina ya wasimamizi
wasaidizi wa uchaguzi mara baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi
wa serikali za mitaa.
Katika
eneo lake, msimamizi wa uchaguzi atatoa maelekezo ya uchaguzi siku
zisizopungua 28 kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni ya 7(1),
8(1) ya kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa,
ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2014.
Aidha
msimamizi wa uchaguzi atateua ofisa wa umma mwenye sifa na uadilifu,
atakayeandikisha na kuandaa orodha ya wapiga kura siku 21 kabla ya siku
ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni 8 na 9 ya Kanuni za Uchaguzi wa
Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.
Uteuzi wagombea
Baada
ya hatua zote hizo za awali kufanyika, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi
atabandika orodha ya wapiga kura mahali pa matangazo ya uchaguzi na
kutunza kumbukumbu zake, baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi na
kufanya uteuzi wa wagombea siku zisizopungua 20 kabla ya siku ya
uchaguzi.
Ratiba
iliyotolewa pia inaonesha kwamba Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, katika
muda wa siku mbili tangu siku ya uteuzi kufanyika, atasikiliza na kutoa
uamuzi katika muda usiozidi siku mbili kwa mapingamizi mbalimbali,
kuanzia siku ya kupokea pingamizi husika.
Aidha
kutakuwepo na Kamati ya Rufaa, ambayo wajumbe wake watateuliwa na
Katibu Tawala wa Mkoa na katika uteuzi wake, Katibu Tawala atazingatia
hali halisi ya watumishi wa umma walioko katika wilaya husika.
Kamati
hiyo ya Rufaa, itateuliwa siku saba kabla ya siku za uteuzi wa wagombea
kwa mujibu wa Kanuni ya 16(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.
Kampeni
Kwa
mujibu wa ratiba hiyo, kampeni za uchaguzi zitafanyika wiki mbili za
mwisho kabla ya siku ya uchaguzi na zitafanyika kwa muda wa siku 14 na
zitamalizika siku moja kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2014.
Ili
kufanikisha uchaguzi huo, wananchi wametakiwa kujiandikisha katika
Rejista ya Wapigakura, itakayoandaliwa siku ishirini na moja kabla ya
siku ya uchaguzi; na uchaguzi utafanywa kwa kutumia karatasi maalumu za
kupigia kura.
Aidha
kura zitapigwa na kutumbukizwa kwenye masanduku ya kupigia kura na kama
kawaida, uchaguzi utafanyika katika ngazi ya kitongoji na mitaa katika
sehemu ya faragha na hakutakuwa na mikutano ya uchaguzi katika ngazi za
vijiji.
Uchaguzi uliopita
Katika
uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa, CCM kilipata ushindi wa
kishindo wa zaidi ya asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa, hatua
iliyochukuliwa na wachambuzi wengi kuwa ni dalili kuwa chama hicho
kilikuwa kinakwenda kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Uchaguzi
wa mwaka huu, mbali na kuendelea kutumika kutoa ishara za uchaguzi mkuu
ujao, pia utakuwa na umuhimu wa ziada katika kupima uimara wa
makubaliano ya vyama vikubwa vya siasa, vilivyounda kundi la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakati wa mchakato wa Katiba mpya na
kukubalika kwao kwa wananchi.
Tayari
viongozi wa vyama hivyo, Chadema, CUF na NCCR Mageuzi, walishatoa kauli
ya kuhoji kwa nini uchaguzi huo unachelewa, wakihofia kuwepo wanachoita
mchezo mchafu wa kuwashitukiza.
Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alinukuliwa akidai Serikali
imeshindwa kutangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo, lakini pamoja
na hitilafu hiyo, chama hicho kimeshatoa taarifa kwa wanachama wake
kujiandaa kugombea.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, alinukuliwa akidai kwa kuwa
uchaguzi huo hufanyika Septemba kila mara na kwa kuwa mwaka huu kuna
Bunge Maalumu la Katiba linalomalizika Oktoba, Serikali ilitakiwa
kulitambua hilo na kutoa ratiba mapema.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema, John Mnyika alisema kutokana na
mchakato wa kupata Katiba mpya kusuasua, vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi vinatakiwa kushirikiana ili kushinda viti vingi.
0 comments:
Post a Comment