MJUMBE ARFI ARUDISHA HOJA ZA UKAWA BUNGENI: SOMA HAPA
Mjumbe wa Bunge Maalumu, Said Arfi
amelitikisa Bunge jana baada ya kuwasilisha hoja sawa na zile
zinazosimamiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Kati
(Chadema), alilitikisa Bunge hilo, alipowasilisha maoni ya wajumbe
wachache wa Kamati Namba 10 inayoongozwa na Anna Abdallah.
Alisema wajumbe wengi wamependekeza
marekebisho ya sura ya saba kwa kuweka Makamu wa Rais watatu yaani
mgombea mwenza, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema wachache
wamependekeza sura hiyo kubaki kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu kwa
sababu muundo wa serikali tatu uliopendekezwa hauhitaji kuwa na makamu
wa rais watatu wala ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Rasimu hiyo, Ibara ya 70
inasema kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano itayokuwa na Rais,
makamu na mawaziri wa Jamhuri ya Muungano.
Tofauti na walio wengi ambao
wamependekeza mawaziri na naibu mawaziri watokane na Bunge, wachache
katika kamati hiyo wametaka ibaki kama ilivyo katika Rasimu ya kuwa
mawaziri wasitokane na wabunge.
Alisema mapendekezo hayo yataleta ufanisi zaidi katika utendaji wa mawaziri katika wizara husika.
“Sababu nyingine ni kuondoa uwezekano wa
waziri ambaye ni mbunge kupendelea jimbo lake la uchaguzi ili aweze
kuchaguliwa tena katika chaguzi zinazofuata,” alisema.
Pia alisema wajumbe wengi wameondoa
dhana ya Serikali ya Tanganyika na kufuta mapendekezo yanayoweka
utaratibu wa viongozi wa serikali hiyo kushiriki katika chombo cha
uhusiano na uratibu wa Serikali kinachoanzishwa na Rasimu.
Hata hivyo, alisema wajumbe wachache
wamependekeza ibara hizo zibaki kama zilivyopendekezwa katika Rasimu ya
Katiba kwa sababu maudhui yaliyowekwa yanakidhi muktadha na majukumu ya
chombo husika katika muundo wa serikali tatu.
Arfi alisema wajumbe wengi walipendekeza
kuingizwa kwa sura na sehemu mpya zilizopendekezwa kuhusu mamlaka ya
umma, ardhi, maliasili na mazingira na sehemu ya Taasisi ya Kuzuia
Rushwa katika sura ya 13.
Alifafanua kuwa wajumbe wengi pia walipendekeza sura ya ardhi, maliasili na mazingira.
“Wajumbe wachache hawazikubali sura na
ibara mpya zote zilizopendekezwa kwani zinalenga katika kuongeza mambo
ya muungano katika Rasimu ya Katiba,” alisema.
Katika kamati hiyo, wajumbe wengi
wamependekeza kuwapo na uraia wa nchi zaidi ya moja kwa sababu
Watanzania walioko nje ya nchi wangependa kurudi na kuwekeza nyumbani
kwao.
Hata hivyo, alisema wajumbe wachache
wamependekeza sura hiyo ibaki kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya
Katiba kwa sababu kuna hatari nyingi zinazoambatana na uraia pacha ikiwa
ni pamoja na kuhatarisha usalama wa nchi.
0 comments:
Post a Comment