728x90 AdSpace

Latest News

Monday, September 1, 2014

Mhe Membe Afunguka: Bila kufuli la CCM pasingetosha urais 2015

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akisisitiza jambo katika mahojiano maalumu na wahariri wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam, hivi karibuni. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Kizitto Noya, Mwananchi
Uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM wa kuwadhibiti kwa mwaka mmoja makada wake sita waliobainika kukiuka kanuni kwa kuanza mapema kampeni za urais, unaweza kuwa uliwakera wengi, lakini si Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ambaye ni mmoja wa ‘waliofungwa kufuli’.
Membe anaona adhabu hiyo ilikuwa mwafaka na kwamba laiti uamuzi huo usingefanywa mapema, “ingekuwa vurugu tupu”.
“Sijui nchi hii ingekuwa wapi kama watu wangeachwa bila ya kuwekewa ‘gavana’,” alisema Waziri Membe kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika kwenye ofisi za wizara hiyo jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Membe pamoja na makada wengine, Frederick Sumaye, Edward Lowassa, William Ngeleja, Stephen Wasira na January Makamba walibainika kukiuka kanuni za uongozi na maadili za CCM kwa kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa na CCM kugombea urais.
Kwa mujibu wa taarifa ya CCM iliyotolewa baada ya kikao cha Kamati Kuu, makada hao walikiuka kanuni za uongozi na maadili za CCM kwa mujibu wa Toleo la Februari 2010 Ibara 6 (7) kwa baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Bila ya kueleza ni jinsi gani vurugu hizo zingefanyika, Membe alisisitiza kuwa vurugu ingekuwa kubwa kama chama hicho kisingechukua hatua mapema.
“We angalia, kuna makundi mawili. Hili kundi letu (la walioanza kampeni mapema wakaadhibiwa) na hili jipya la hawa ambao wameanza kujitokeza sasa, ingawa najua nao watadhibitiwa tu. Hawa wasingedhibitiwa, ingekuwaje?” alihoji Membe.
Wakati CCM inawaita makada hao kwa ajili ya kuwahoji, tayari baadhi walishaanza kufanya sherehe na kualika wenyeviti wa mikoa ambao walieleza misimamo yao juu ya mgombea urais wanayemuunga mkono, wengine kuzunguka kwenye hafla mbalimbali kwa ajili ya harambee na wengine kuzigawa jumuiya za chama hicho, hasa Umoja wa Vijana (UVCCM), huku baadhi ya vikao vikiripotiwa kutawaliwa na malumbano yaliyosababishwa na misimamo tofauti kuhusu mgombea urais wa CCM.
Hata hivyo, Waziri Membe (61) hakusita kukosoa muundo wa vyombo vya uamuzi vya CCM ambao unawapa fursa baadhi kushiriki katika kuadhibu wanaotaka nafasi fulani na baadaye walioadhibu kujitokeza kuwania nafasi hiyo akisema utaratibu huo unawaonea wale ambao hawana fursa ya kuwadhibiti wengine.
“Chama chetu sasa kiwe na utaratibu unaowabana watu fulani kugombea kutokana na nyadhifa zao. Kwa mfano, uko kwenye nafasi ya kufanya uamuzi, unawaadhibu hawa halafu baadaye unajitokeza wewe. Huwezi kuchuja halafu ukajitokeza wewe (kugombea). Kutakuwa hakuna objectivity (haki),” alisema bila ya kuweka bayana watu waliohusika katika kuadhibu na baadaye wakajitokeza kuwania urais.
“Tuwe na utaratibu kwenye chama kwamba wanaowabana watu fulani, wasigombee na hasa wale walioshiriki uamuzi ule na wengine walioko kwenye nafasi za uamuzi… Kamati Kuu na hata (Halmashauri Kuu) Nec na Kamati ya Maadili, nao wasije kujitokeza baadaye na kutangaza nia. Vinginevyo hatutawaelewa,” alisema.
Pamoja na kusifu kitendo cha Kamati Kuu kudhibiti makada mapema, Membe anaona muda umefika kwa CCM kuruhusu wanachama wake wanaowania urais waanze harakati zao sasa.
“Huu ndiyo msimu wenyewe,” anasema Membe ambaye alizungukwa na wasaidizi wake wakati wa mahojiano hayo.
“Kinachotakiwa sasa ni chama kitoe guidelines (miongozo) kwa wagombea. Kiseme wanapaswa kufanya moja, mbili, tatu…. Chama kiruhusu, lakini wagombea wasivuke mipaka hiyo iliyowekwa.”
Kuhusu ndoto yake
Waziri Membe, ambaye alikuwa makini kutotamka waziwazi uamuzi wake wa kugombea urais mwakani, alisema amekuwa na ndoto siku nyingi na alianza kuipima ndoto yake hiyo katika uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mwaka 2012 alipogombea nafasi hiyo kupitia kundi aliloliita “la kifo”.
“Ningeweza kuingia Nec kupitia nafasi ya wilaya ambako kwa vyovyote sikuwa na mpinzani. Lakini niliamua kwa makusudi kupima kukubalika kwangu ndani ya CCM. Katika kujipima huko, nikaamua kugombea nafasi hiyo katika ngazi ya taifa. Sasa kuna watu waliojua ndoto yangu na wakataka kunidhibiti. Wakatumia mabilioni kuniharibia ili kuhakikisha sipiti. Waliamini kwamba ningeangushwa, nisingeweza kurudi tena hapo kuomba nipitishwe,” alisema Membe.
“Kwangu ilikuwa ni vita kuu… nilikuwa kwenye kundi la kifo. Sikufanya kampeni, sikutumia hela wala ushawishi wowote, lakini niliwashinda watu 26. Katika kundi lile (la watu 32), mimi ni mgombea pekee ambaye si mjumbe wa sekretarieti na wala sikuwa mjumbe wa Kamati Kuu. Sikwenda mikoani kutafuta kura wala sikutoa chochote.”
Membe anaongeza kusema: “Nilitaka kupima kama uadilifu wangu ungeweza kunipa nafasi ya uongozi ndani ya chama. Nilikuwa mjumbe pekee aliyepigwa vita kali na makundi yote. Mabilioni ya fedha yalichangwa na wajumbe kuagizwa wasimchague Membe. Mlishuhudia jinsi kina (jina tunahifadhi) walivyonitukana, lakini nikashika nafasi ya sita. Kati ya kura 2011, nilipata kura 1,455 sawa na asilimia 77.”
Alipoulizwa haoni kama mabilioni hayo ya fedha yaliyochangwa kwa ajili ya kuhonga wajumbe, yanadhihirisha kwamba chama hicho kimetawaliwa na rushwa, Membe alikuwa nadhifu katika kuisafisha CCM.
“Mkutano mkuu uliondokana na kashfa ya rushwa kwa ajili yangu. Ni fact (ukweli) kwamba wale watu waligawa rushwa, wajumbe walichukua wakatafuna, lakini hawaku – comply (hawakufuata masharti ya watoaji rushwa),” alisema.
Makundi ya urais
Kila wakati uchaguzi mkuu unapokaribia, CCM hugawanyika katika makundi kulingana na mtazamo wao kwa wagombea urais kwa tiketi ya chama hicho, kiasi cha kutishia kusambaratika. Hali hiyo huwafanya baadhi kuona kuwa ni bora mgombea asiye na makundi ndiye apitishwe kukinusuru chama kusambaratika. Lakini Membe ana mtazamo tofauti.
“Asiwadanganye mtu. Hakuna mgombea urais duniani asiyekuwa na makundi na akitokea mgombea huyo (asiye na makundi), basi ni dhaifu. Kuwa na makundi ni potision (msimamo). Makundi katika uchaguzi ni muhimu kwa kuwa yanamtofautisha mgombea mmoja na wengine. Kimsingi, makundi ndiyo msimamo wa mgombea.
“Mfano kama ni suala la ushoga, uko wapi; kama ni ufisadi, uko kwenye kundi gani. Huwezi kuwa katikati. Ukiwa katikati maana yake ni kwamba nusu unaunga mkono ushoga na nusu hauutaki. Utakuwa hueleweki.
“Kama kuna mambo huyataki, hayo ndiyo yanayo – define (yanayoelezea) kundi lako. Mfano kama (Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph) Warioba anataka serikali tatu na mimi nataka serikali mbili, haya ndiyo makundi yetu. Wote ni CCM, lakini tuna makundi tofauti.”
Sifa za urais
Kuhusu mtazamo wake juu ya sifa za mgombea, Waziri Membe alisema urais ni taasisi nyeti mno watu kuigombea. “Mtu huwezi kusema nagombea urais ili nitekeleze ilani ya chama. Lazima uwe na mambo ya msingi kabisa ya kuwaambia watu kwa nini unataka urais. Huwezi kugombea urais eti kwa sababu una hela za kuwapa watu ili wakuchague,” alisema.
“Tunaweza kuweka sifa 100 au hata 300 za urais, lakini sifa za msingi kabisa za kiongozi huyo ni uchapakazi wake hapo alipo na siyo zamani. Pia tunaangalia uadilifu wake na anachotaka kutufanyia Watanzania. Mgombea urais lazima uende beyond (mbali na) ilani ya chama. Hata mbunge na diwani hutekeleza ilani ya chama! Sasa kwani ni lazima utekeleze ilani ya chama ukiwa Ikulu? Lazima ueleze utafanya nini.
Atagombea urais mwakani?
Membe amesema ana ndoto ambayo bado anaitafakari kuona maana yake. “Ndoto ziko za aina mbili; ile ya mtu kulala akaota na ikabainika kuwa ya kweli na ndoto ambayo ni people driven (inayotokana na maoni ya watu).
Akifafanua alisema, ndoto inayotokana na ushabiki wa watu ni ya kujipima na katika siasa mtu hawezi kujipima mwenyewe. Unahitaji timu kwa ajili ya utafiti wa uwezo wako na changamoto unazoweza kukumbana nazo katika hiyo ndoto, alisema.
“Hata wakati unapopata ushauri wa watu hao, bado haujaoteshwa. Ni process (mchakato). Hukurupuki tu. Huwezi kusema unataka, halafu uje uharibu nchi ya watu. Si suala la haki ya kikatiba. Mtu unaulizwa kwa nini unagombea, unajibu ‘ni haki yangu ya kikatiba’. Ah! Wewe mpuuzi? Ni lazima upate watu wa kukushabikia.
“Nchi ya watu milioni 45, ina watu wengi wenye akili sana, hivyo lazima ujiulize ‘why me? ( kwa nini mimi?)Wewe una nini zaidi mpaka uitake nafasi hiyo. Kusubiri kuoteshwa ni pale wenzako wa kweli wanaposema wamepima kukubalika kwako.”
Alipoulizwa kama tayari ameshaunda timu inayofuatilia na kuchunguza ndoto yake hiyo alijibu, “Ipo na nadhani mwezi ujao itaniletea majibu”.
Waziri Membe tayari ametangaza kutogombea tena ubunge katika Jimbo la Mtama mwaka 2015 na alipoulizwa anapanga kufanya nini baada ya hapo alijibu: “Tofauti na wengine, kwangu ubunge siyo kazi ya kudumu. Nilishawaambia kwamba sitagombea tena na nimewapa ruksa watu kuanza kujipitisha jimboni kwangu, sina tatizo nao.”
Waziri wa Mambo ya Nje na urais
Kwa miongo miwili, watu walioshika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ndiyo waliopitishwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM na wakashinda. Benjamin Mkapa alishika wizara hiyo kabla ya mwaka 1995 kuwa Rais na baadaye mrithi wake, Jakaya Kikwete alishika wizara hiyo kwa miaka 10 na sasa ni Rais.
Hata hivyo, Membe hadhani kama kushika nafasi hiyo ni kujihakikishia urais… “Siyo ajabu Waziri wa Mambo ya Nje akashindwa urais, lakini marais wengi sana duniani wametokana na nafasi ya uwaziri wa mambo ya nje. Kama nilivyowaambia, mimi ni waziri wa 13 kushika wizara hii, lakini si wote wamekuwa marais.”
Hata hivyo, alisema waziri anayeshika wizara hiyo ana sifa za ziada kutokana na ukweli kuwa anakuwa na uzoefu katika masuala ya uongozi na itifaki katika ngazi ya kimataifa.
“Sifa ya kiongozi wa nchi ni kuwa connected to the world (kuwa umeunganishwa na dunia). Smart people (watu makini) hawachagui kiongozi ambaye hayuko connected,” alisema na kuongeza kuwa kutokana na kuongoza wizara hiyo anakutana na viongozi mbalimbali duniani, wawekezaji, wafanyabiashara na kufahamu kwa kina masuala ya ushirikiano.
“Rais huendi kujitambulisha kwa wenzako, lazima uwe unajua baadhi ya mambo. Haiwezekani wewe kila kitu unajifunzia Ikulu, kuapisha viongozi, kusoma hotuba, kukaribisha wageni ujifunze kwenye kipindi chako cha uongozi. Sasa hizo ndizo kazi za kila siku za waziri wa mambo ya nje,” alisema.
“Kazi zangu zote mimi (Wizara ya Mambo ya Nje) ni maagizo ya Rais na wizara hii ni idara ya Rais. Ni mkono wa Rais, hivyo ukiwa hapa una picha nzuri ya uongozi wa nchi. Lakini kama nilivyosema hata hivyo, siyo automatic (moja kwa moja), chama kinapaswa kukuchagua na watu wakukubali.”
CHANZO;MWANANCHI
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: Mhe Membe Afunguka: Bila kufuli la CCM pasingetosha urais 2015 Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top