728x90 AdSpace

Latest News

Monday, September 22, 2014

ASKOFU KKKT APINGA MCHAKATO WA KATIBA MPYA MBELE YA MIZENGO PINDA

Askofu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Ambele Mwaipopo ametaka kusitishwa kwa mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya kwa kuwa Bunge la Katiba limepuuza maoni ya Watanzania yaliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

Askofu Mwaipopo alisema hayo jana kwenye ibada ya kusimikwa kuwa askofu wa kanisa hilo, katika Kiwanja cha KKKT, Usharika wa Sumbawanga Mjini, iliyohudhuriwa viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

“Tusione aibu kujikosoa kama tumekosea...zoezi hilo lisitishwe ili tujipange upya lakini kuendelea kupuuza maoni ya Watanzania itatugharimu,” alisema Askofu Mwaipopo huku akishangiliwa na waumini.

Alisema kanisa hilo litaendelea kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kusaidia kupatikana kwa viongozi wenye nia ya kuboresha maisha yao na kuondoa wanaosababisha umasikini.

“Nchi hii ni tajiri, ina rasilimali nyingi, umasikini unatokana na kuwa na viongozi wanaojijali wenyewe badala ya kuangalia maisha ya Watanzania wote...sasa tutahakikisha tunahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili watuchagulie viongozi safi,” alisema.

Awali, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Alex Malasusa alitaka viongozi wa Taifa kubadilika na kuwa na dhamira ya kutenda kile wanachokizungumza kwa kuwa wamekuwa mabingwa wa kuongea kuliko kutenda.

Dk Malasusa alisema viongozi wamekuwa mstari wa mbele kuzungumzia rushwa wakati hawana dhamira ya kupambana nayo, hivyo imefika wakati matendo yao yaendane na kauli zao.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Pinda alisema mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya unaondelea ni halali kwa kuwa Bunge hilo lipo kisheria na haliwezi kusitishwa, kinachofanyika ni kuboresha yaliyomo kwenye Rasimu iliyowasilishwa kwao.

“Walioandaa ile Rasimu ni binadamu kama sisi, kuna mambo mengi waliyasahau, sasa tunayaboresha.

“Hatuwezi kupitisha vilevile ile Rasimu, wananchi wangetushangaa kulikuwa na upungufu mwingi kama kwenye ardhi, haki za binadamu na za walemavu,” alisema Pinda.

Alisema kama tatizo ni muundo wa muungano anafikiri kuna haja ya wananchi kupiga kura ya maoni kama wanataka muungano wa aina gani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: ASKOFU KKKT APINGA MCHAKATO WA KATIBA MPYA MBELE YA MIZENGO PINDA Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top