TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
“Demokrasia bila mipaka ni ukichaa na demokrasia bila nidhamu ni uwendawazimu” Mwl Jk Nyerere
Ndugu
zangu Watanzania, naomba mfahamu kuwa miongoni mwa wajumbe wote wa
bunge la katiba takriban 600, wajumbe waliofanya maamuzi haramu ya
kugomea ni 79 ambao ni pungufu ya asilimia 15% ya wajumbe wote, na sio
kweli kuwa wao pekee ndio wenye tafsir sahihi ya rasimu. Wajumbe wa
makundi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa vyama vyote vya siasa
takriban 18 kati ya 22 bado wamo kwenye bunge, kati ya wajumbe wa kundi
la 201 walioasi ni 15 ambapo bara ni 9 na zanzibar 6 lakini pia katika
wanaojiita UKAWA wapo wabunge ambao wameendelea kurudi bungeni kwa
kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Takwimu hizi zinatuthibitishia kuwa
UKAWA ni kikundi kidogo cha watu waliojipanga kuvuruga AMANI ya nchi,
watu ambao hawataki KATIBA wala hawataki MUUNGANO.
Ndugu
zangu watanzania, naomba leo niwape picha na kilichopo nyuma ya pazia
ya kikundi hiki kiitwacho ukawa ambacho kinaratibiwa na viongozi
wachache na maslahi yake kujulikana kwa wachache zaidi tena yaliyojikita
katika misingi ya kibinafsi. Mfano, ndoa ya CUF na CHADEMA inayopelekea
NCCR mageuzi kuwa bendera fuata upepo imejengwa katika misingi ya
kuvunja muungano, kwa makubaliano kuwa CUF kubaki na Zanzibar na CHADEMA
kubaki na Tanganyika. CUF inataka inufaike na mkakati dhalimu wa
kunyonya rasilimali za wazanzibar yakiwemo mafuta bila kushurutishwa na
sheria za muungano kwani wakiamini kubaki na muungano imara CUF na
viongozi hao wachache katika chama hicho wanakosa fursa za kupora
rasilimali za wazanzibar. Ikubumbukwe Muungano ndio unalinda mipaka na
usalama wa raia katika kujiendeleza na kujinufaisha bila ubaguzi wa
kikundi cha watu wachache ambacho kinaenda kinyume na utawala wa sheria.
Ikumbukwe
kuwa rasimu ya CUF walioipeleka kwa Mhe. Raisi mwaka 2011, mapendekezo
yao ni tofauti na madai yao sasa ya serikali 3, hapa inatosha kutupa
picha kuwa nia yao ni kuvunja muungano ili watuache katika mfarakano
kama nchi nyingine zinazoteseka kwa sababu ya wanasiasa uchwara.
Ifahamike
ajenda ya CHADEMA ni kuvunja muungano ndio maana CHADEMA hawahangaiki
kuimarisha chama Zanzibar, nia yao ni kubaki na Tanganyika ili waigawe
Tanganyika katika vipande vipande kwa lugha ya majimbo ili adhima yao ya
ukanda na ukabila itimie. Moja ya kanda yao ambayo wametangaza katika
kanda 8 walizo nazo ni Kilimanjaro, tanga, arusha na manyara. CHADEMA
ina amini kanda hii inajitosheleza kwani ina bandari,bunga za
wanyama,madini, milima . Na hii imepelekea mbunge mmoja wapo wa CHADEMA
kulazimika kusema kaskazini ni nchi huru huku mwenyekiti wao Mbowe
akiendelea kudai mapato ya mlima Kilimanjaro yabaki Kilimanjaro.
Katika
kipindi hiki ambacho wenzetu wamegomea bunge la katiba ambalo lipo
kisheria na madai yao yakibadilika kila kunapokucha tena yakiwa na
upotoshaji mkubwa kwa kufanya siasa chafu ili mradi watimize azma ya
kuisambaratisha Tanzania wakiwa makuwadi wazuri wa soko huria. Ukihoji
leo sababu iliyowafanya watoke bungeni ni tofauti kabisa na sababu
waliyoitoa siku wanatoka bungeni, eti msingi wao mkuu wao ni watetezi wa
wananchi. Lakini tumesikia katika vyombo mbalimbali wananchi hao
wakiwaasa na wakiwataka warejee bungeni ili kukamilisha kazi ya kisheria
na tumaini la watanzania la kuwapatia katiba mpya. UKAWA hawa bila haya
wamekataa. Swali..? wanamtumikia nani. Mpaka sasa imepelekea wananchi
hao wanaosema wanawawakilisha wameamua wenyewe kuja Dodoma kuendelea
kusema kero zao na shida zao ili katiba hii iweze kutoa majawabu, mfano
tumeshuhudia makundi ya wakulima, jukwaa la wahariri wa vyombo vya
habari, wafugaji na makundi kadha wa kadha yameendelea kutiririka
Dodoma. Hii ni picha tosha kuwa UKAWA hawawatumikii watanzania na
wameamua kuwahadaa watanzania kwa mgongo wa kuwatetea huku ajenda yao
ikiwa maslahi binafsi.
Ndugu
zangu watanzania tunapowaunga mkono watu wanaoendelea kuligomea bunge
la katiba wakati tunajua nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria, na wao
ndio wamevunja sheria, tujue kabisa kuwa tunaenda kinyume na utawala
bora, ambao umejengwa kwenye msingi wa sheria na demokrasia. Msingi wa
demokrasia sio kususa baada ya kushindwa hoja, UKAWA hawataki hoja za
wengine na wanalazimisha hoja zao pekee ndizo zikubalike kinyume na
msingi wa demokrasia. Na bila haya watu hao wasiojua demokrasia
wameendelea kuwashawishi watanzania waingie barabarani huku wakijua kuwa
Katiba haipatikani barabarani kama wanahoja kwanini wanaikimbia
Dodoma..? Mchakato huu ulianza kisheria na utahitimishwa kisheria, sio
matamko ya makuwadi wa soko huria.
Miongoni
mwa madai yao matatu, (i) Rais avunje bunge (2) kinachojadiliwa Dodoma
sio rasimu ya warioba (3) Serikali tatu ndio maendeleo
Kwa
ujumla wake, UKAWA wanajua mamlaka ya Rais kwa mujibu wa sheria ya
mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011, sura namba 83 imempa Rais mamlaka ya
kuunda tume, kuchagua wajumbe 201, kutangaza na kuitisha bunge na
kuzindua bunge la katiba, kupokea katiba inayopendekezwa na kuitangaza
kwenye gazeti la serikali.,kwanini wanataka kumlazimisha Rais kuvunja
Sheria kwani hayo niliyoyataja ndio ambayo Rais anayo mamlaka ya
kisheria kuyafanya katika mchakato huu wa Bunge la Katiba, na ndio maana
hata wale wajumbe aliowateua ambao wamegomea Rais
hajawatengua.,kinachojadiliwa bungeni ni Rasimu ya jaji warioba na kiko
wazi, kwa sababu msingi mkuu wa majadiliano ni Rasimu inayotokana na
tume tena kwa mujibu wa Sura namba 83 kifungu cha sheria namba 25/26 na
kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu namba 33 (8). Wanajua mamlaka ya
bunge na waliohusika kutengeneza sheria hizi pamoja na kanuni waache
kuwahadaa watanzania.
Jambo
la mwisho lenye kusikitisha zaidi ni kung’ang’ania Serikali tatu kana
kwamba ndio kilio kikubwa cha watanzania, naomba niulize swali kati ya
Muungano na migogoro ya ardhi ni jambo lipi limepoteza maisha ya
watanzania wengi na ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi ili watanzania
wasiendelee kumwaga damu. Kati ya tatizo la ajira na muungano, kati ya
afya na muungano, kati ya maji salama na safi na muungano, kati ya elimu
bora na muungano, kati ya haki za binadamu na muungano eti watu hawa
wanaojiita ukawa kwao muhimu muungano kuliko chochote kile.
Watanzania naomba tupime kama ni kweli kuwa hawa ni watetezi wetu au ni makuwadi wa soko huria.
Kwa
niaba ya watanzania wazalendo, napenda kuiomba serikali kupitia vyombo
vyake vya ulinzi na usalama kuwatupia UKAWA jicho la pekee katika
kuangalia na kufuatilia kwa ukaribu zaidi nyendo za UKAWA na hata
kutuambia ni nani wako nyuma yao kiasi cha kuwa na kiburi cha
kupindukia. Wito wa watanzania kwa vyombo vya ulinzi na usalama ni kuwa
amani, umoja na uhai wa nchi hii uko mikononi mwao, kwani nia ya UKAWA
sio nzuri kwa mustakabali wa taifa hili na lazima wakumbuke USIPOZIBA
UFA UTAJENGA UKUTA na pia MAJUTO NI MJUKUU NA HUJA BAADAE. UKAWA
wanataka kutengeneza Misri, Afrika ya Kati, Libya, Syria, Sudani Kusini
nyingine hapa Tanzania.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Katibu , idara ya Hamasa na chipukizi
Jumuia ya vijana chama cha mapinduzi (UVCCM)
0 comments:
Post a Comment