Katika
vurugu hizo, Makonda anatuhumiwa kumpiga aliyekuwa Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.
Amesema hawezi kumfanyia kitendo kama kile Jaji warioba kwani anamuheshimu kama mzazi wake.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo, Makonda amesema kimsingi hahusiki na vurugu hizo wala
kumpiga mzee Warioba kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.
Makonda amewaambia waandishi wa habari kuwa tofauti na uzushi huo,
yeye alishiriki kwa kiasi kikubwa kuepusha mzee Warioba asipigwe na
vijana waliokuwa wanashiriki vurugu hizo na kwamba bado ana uhusiano
mzuri na mwanasiasa huyo mkongwe nchini.
"Jaji Warioba ni mzee wangu na tumekuwa tukishirikiana katika mambo
mengi na ya msingi yanayohusu mustakbali wa nchi..haitakuwa jambo la
kawaida kwa mimi kumdhuru mzee Warioba na kwamba katika kuthibitisha
ukweli huo, tangu baada ya tukio hilo nimekuwa nikiwasiliana naye na
tumekuwa tukipeana pole kwa yaliyotokea jana." amesema Makonda.
Ameongeza kuwa wanaozusha uvumi huo ni watu wenye nia ovu juu yake na
ambao wanadhani kwa kufanya hivyo watamzima kisiasa, ambapo yeye
mwenyewe amesema hajui walioanzisha vurugu hizo walikuwa na nia gani
kwani hawaoneshi kuwa na msukumo wa chama chochote cha siasa.
Mwanasiasa huyo kijana amewataka wale wote wenye hisia potofu juu ya
nani hasa mhusika wa vurugu hizo kwenda kuonana na uongozi wa ukumbi wa
Ubungo Plaza ili wapatiwe picha za kiusalama za CCTV ambazo zitaonesha
chanzo na nani hasa amehusika na vurugu hizo.
Aidha, ameongeza kuwa wakati vurugu hizo zinaanza, muda mwingi
aliutumia kumuokoa mmoja wa washiriki ambaye ni mlemavu wa macho pamoja
na Jaji Warioba, lakini cha kusikitisha ni kwamba watu wenye nia mbaya
wanatumia nafasi hiyo kutaka kumchafua kwa faida za malengo yao ya
kisiasa.
Baraza la Wazee la Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania limelaani
vikali kuvamiwa hapo jana kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba nchini Jaji Mstaafu Joseph Warioba wakati akiwa katika
mdahalo wa Katiba inayopendekezwa uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo
Abdallah Tambagwaza na Katibu Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Dar
es Salaam Mohamedi Ligola wamesema vijana wana wajibu wa kuheshimu
mawazo ya wazee na hawapaswi kuwadharau kwani kufanya hivyo ni kwenda
kinyume na maadili ya nchi.
Wazee hao wamesema hata katika Bunge Maalum la Katiba kulikuwa na
baadhi ya wajumbe walikuwa wakipingana na mchakato wa bunge lilivyokuwa
linaendeshwa lakini kulikuwa na njia bora zilizotumika katika kuleta
maridhiano na si vurugu kama ilivyotokea hapo jana.
0 comments:
Post a Comment