BAMAKITA wampongeza Mwigulu, waibana UKAWA
BARAZA
la Maadili la Kiislamu nchini (BAMAKITA), limeunga mkono kauli
iliyotolewa na Mbunge wa Iramba Magharibi, mkoani Singida, Bw. Mwingulu
Nchemba kutaka vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, viahirishwe ili kuokoa
fedha za walipakodi nchini.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa baraza hilo,
Shekhe Athuman Mkambaku, alisema kauli ya Bw. Nchemba inaonesha ni
mzalendo halisi anayelipenda Taifa lake.
Alisema hivi karibuni,
Bw. Nchemba alishauri Bunge hilo liahirishwe kwani wajumbe waliopo
hawawezi kuwapatia Watanzania Katiba Mpya kutokana na theluthi mbili
inayotakiwa kwa mujibu wa sheria, haiwezi kupatikana kwa sababu baadhi
ya wajumbe kutoka upinzani hawashiriki vikao vya Bunge hilo.
"Kuendelea kuwalipa
posho wajumbe wa bunge hili ni matumizi mabaya ya fedha za
umma...Nchemba ameonesha ukomavu wa kisiasa na maneno yake hayapaswi
kupingwa wala kupuuzwa bali aungwe mkono na kupongezwa," alisema.
Aliongeza kuwa, baraza
hilo linapinga vikali kitendo cha baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba
kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kuendelea kususia
vikao wakiamini pengine wanatumiwa na kundi la watu wasiotaka Katiba
Mpya ipatikane.
"Hoja za UKAWA
zilizowafanya wagomee vikao hivyo hazina mashiko kwani wao wanataka
rasimu ipite kama ilivyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba...kama madai yao ni sahihi, kwa nini waende bungeni kuchukua
posho tu?" alihoji.
Alisema lazima wajumbe wa Bunge hilo wabadili baadhi ya vifungu, waongeze na kuviboresha ndio maana ya vikao.
Shekhe Mkambaku wajumbe
kutoka umoja huo hawapaswi kugoma kwa hofu kwamba, Katiba Mpya
itatengenezwa kulingana na matakwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kutokana na wingi wao bali watambue kuwa, chama hicho si waamuzi wa
mwisho kwani mwisho wa siku rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi ambao
ndio waamuzi wa mwisho.
"Kama rasimu hii
itatoka kinyume na tulivyopendekeza, wananchi wataikataa, hivyo UKAWA
wasijipe kazi ambayo si yao...kazi hiyo waiache kwa wananchi waitolee
majibu kwa kupiga kura ya kuikataa au kuikubali," alisema.
Baraza hilo pia
limewapinga watu wanaomshambulia Rais wa Jakaya Kikwete wakidai
amevuruga mchakato huo kutokana na hotuba yake alipolihutubia Bunge la
Katiba kwani alichokisema ni ushauri tu.
"Kama Kiongozi Mkuu wa
nchi, bado ana fursa ya kushauri si lazima wajumbe kufuata maoni yake
ndio maana baada ya hotuba yake, vikao viliendelea," alisema Shekhe
Mkambaku.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment