728x90 AdSpace

Latest News

Monday, May 18, 2015

Pinda aainisha mafanikio ya Serikali ya JK kwa miaka 10

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwasilisha bungeni hotuba ya mwelekeo na malengo ya makadirio ya matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2015/2016, bungeni Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana aliwasilisha Bajeti ya lala salama ya ofisi yake na taasisi zake kwa mwaka 2015/16, huku akieleza mafanikio katika sekta mbalimbali yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Nne tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005.
Bajeti hiyo iliwasilishwa katika mkutano wa 20 wa Bunge la 10 ambao ndiyo wa mwisho kwa Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya Bunge kuvunjwa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Akitumia saa 2.30 kusoma hotuba hiyo ya kurasa 105, Pinda alisema katika mwaka 2015/16, ofisi yake imepanga kutumia Sh5.8 trilioni ambazo matumizi yake yatafafanuliwa katika bajeti za wizara zilizopo chini ya ofisi yake.
Pinda alitumia fursa hiyo kuzungumzia pamoja na mambo mengine, mafanikio katika usafirishaji wa reli, bila kugusia harufu ya ufisadi katika ununuzi wa mabehewa katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) uliosababisha vigogo wake watano kusimamishwa kazi.
Mafanikio ya Serikali
Pinda alisema tangu 2005 hadi 2014, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kwamba Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 7,159 yenye thamani ya Dola za Marekani 74,274 milioni na kutoa ajira 869,635.
Alisema katika kipindi cha miaka 10, Serikali iliwawezesha wananchi kubaini fursa za kiuchumi kupitia mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuongeza ajira ulioanzishwa mwaka 2006, kutoa mikopo ya masharti nafuu ya Sh50 bilioni iliyotolewa kwa wajasiriamali 74,790.
"Katika mwaka 2015/16, Serikali itaendelea kuwahamasisha wananchi kuanzisha na kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali, vyama vya kuweka akiba na kukopa ili waweze kukopesheka," alisema. Kuhusu ajira, alisema vijana walioajiriwa katika sekta ya umma ni 188,087 na walioajiriwa katika sekta binafsi ni milioni moja wakati vijana milioni 15 wamejiajiri katika shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara ndogondogo.
Alisema viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka 22 mwaka 2005 hadi 74 mwaka huu.
Kuhusu uchumi, Waziri Mkuu alisema umekua kutoka asilimia 4.7 mwaka 2006 hadi asilimia saba mwaka 2014 na hivyo kuongeza pato la Mtanzania kutoka Sh360,865 mwaka 2005 hadi Sh1.7 milioni mwaka 2014.
"Uzalishaji wa mazao ya uvuvi umeongezeka kutoka tani 341,109 mwaka 2006 hadi tani 375,158 mwaka 2015. Tani 43,354 za mazao ya uvuvi na tani 42,100 za samaki hai wa mapambo ziliuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa Sh7.5 bilioni. Viwanda vya kuchakata samaki vimeongezeka kutoka 25 hadi 48," alisema Pinda. Pia, alizungumzia pia sekta ya utalii akisema idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 1,095,884 mwaka 2013 hadi 1,102,026 na kuongeza mapato ya utalii kutoka Dola za Marekani 1,853 milioni hadi Dola 1,983 milioni.CHANZO:MWANANCHI
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: Pinda aainisha mafanikio ya Serikali ya JK kwa miaka 10 Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top